Kabla ya chanjo yako

Maelezo au taarifa zifuatazo zimetengenezwa kwa ajili ya tovuti hii na wataalamu wa tiba na afya ya jamii kwa kutumia vyanzo au taarifa kutoka katika serikali ya Canada na vingine vya kisayansi na tiba. Hayajakusudiwa kuwa ushauri wa kitabibu. Mara zote unashauriwa kupata ushauri kutoka kwa watoaji huduma ya afya waliofuzu ukiwa na maswali yoyote kuhusu chanjo ya COVID-19 (UVIKO-19).

Ndiyo, watu ambao hapo awali walikuwa na COVID-19 bado wanapaswa kupewa chanjo kamili ya dozi mbili. Wataalam bado hawajui ni kwa muda gani utakuwa umelindwa dhidi ya kuugua ugonjwa huo tena baada ya kupona COVID-19. Chanjo itakusaidia kukukinga kwa kuunda kingamwili za kukabiliana na ugonjwa bila ya kuwa mgonjwa.

Ikiwa hivi majuzi umekuwa na COVID-19, unapaswa kusubiri hadi upate nafuu na uhakikishe kipindi chako cha kujitenga kimepita kabla ya kupokea chanjo.

Ikiwa ulipokea chanjo ya mRNA (Pfizer-BioNTech au Moderna) kama dozi yako ya kwanza, utapewa chanjo ya mRNA kama dozi yako ya pili. Inapendekezwa kuwa upokee chanjo ya aina ileile kama uliyopewa mara ya kwanza, isipokuwa iwe haipatikani kwa urahisi au haijulikani, katika hali hiyo ni sawa kupokea aina nyingine ya chanjo ya mRNA. Zote mbili ni salama na zinafanya kazi vizuri.

Ikiwa ulipokea AstraZeneca kama dozi yako ya kwanza, unaweza kuchagua kupata AstraZeneca kama dozi yako ya pili, lakini NACI sasa inapendekeza uchukue chanjo ya mRNA kama dozi yako ya pili.

Chanjo zote zilizoidhinishwa kutumiwa nchini Canada kwa usawa na kwa ufanisi hupunguza kulazwa hospitalini na ugonjwa mbaya, na zote zina ufanisi wa karibu 100% katika kuzuia kifo kinachotokana na COVID-19.

Jambo muhimu ni kwamba hupaswi kusubiri kupata chanjo ya dozi mbili kwa ulinzi kamili. Aina mpya za virusi zinaibuka ambazo zinasababisha visa vingi, kulazwa hospitalini na vifo, na watu wengi kupata chanjo ndio njia pekee ya kukomesha visa hivi.

Kila mtu anayepatiwa chanjo bado atahitajika kufuata miongozo ya afya jamii. Baada ya kupata chanjo, itakuwa muhimu mno kuendelea kuchukua tahadhari, ikiwemo kuosha mikono, kutokaribiana sana na wengine, kuvaa barakoa na kukaa nyumbani ikiwa unaumwa. Kuna sababu kadhaa kwanini hili ni muhimu:
Inachukua sio chini ya wiki mbili kwa mwili wako kupata ulinzi au kinga kutokana na chanjo ya COVID-19(UVIKO-19). Hii inamaanisha kwamba ikiwa ulipata au uliambukizwa COVID-19(UVIKO-19) kabla ya kupatiwa chanjo, au ndani ya kipindi cha wiki mbili kufuatia chanjo, bado unaweza kuugua COVID-19(UVIKO-19). Kwa hiyo kama utahisi au kuwa na dalili za COVID-19(UVIKO-19) baada ya kuwa umeshapatiwa chanjo, nenda kapimwe.
Chanjo haitomzuia kila mtu kupata au kuambukizwa COVID-19(UVIKO-19). Kwa wale ambao watapata au kuambukizwa kirusi, kuna uwezekano mdogo sana kwa wao kuugua sana.
Chanjo zilizopo ni madhubuti sana lakini unaweza kuwa kwenye kundi dogo la watu ambao hawana kinga. Bado unaweza kusambaza COVID-19(UVIKO-19) ikiwa utawasiliana au kuingiliana kwa karibu na watu au hutofuata masharti au hatua za udhibiti za afya jamii.

Hapana, kupatiwa chanjo ya COVID-19(UVIKO-19) ni hiari yako kabisa. Ni chaguo lako aidha kupata au kutopata chanjo ya COVID-19(UVIKO-19).

Wakazi wote wa Canada, bila kujali hali zao za uhamiaji, wanastahiki kupatiwa chanjo ya COVID-19(UVIKO-19). Huhitaji kuwa na kadi halali ya huduma za afya (PHN). Hivi sasa, watu wenye umri wa miaka 19 na kuendelea ndio pekee wanaostahiki kupata chanjo za Moderna, AstraZeneca na Johnson & Johnson. Watu wenye umri wa miaka 12 na kuendelea wanastahiki kupata chanjo ya Pfizer-BioNTech.